Simulizi: JIRANI KAMA JIRANI!



Imeandikwa na: Abyas Mzigua 


Sehemu ya pili


ILIPOISHIA:

 Mke wangu aliondoka nyumbani. Akaniacha mwenyewe. Mchana jirani yangu akaja na kuniletea chakula, pamoja na kujitahidi kukikataa kwa kumueleza nimekwisha kushiba, bado alinilazimisha na kuniambia nikihifadhi nitakula usiku. Hapo sikuweza kumpinga. 


Sasa tuendelee!


  Kama ambavyo niliwaeleza, lile poti la chakula nililipokea na kuliingiza ndani. Nikaliweka mezani na kurejea kwenye usingizi wangu. Nilikuja kushtuka kagiza kanakaribia kuingia. Nikagundua kuwa usingizi wangu ulikuwa ni mrefu sana. Ni kweli nilichoka, mno. Usiku wa jana yake sikuwa nimepata usingizi wa kutosha. Nilikuwa ninafanya kazi ya kumbembeleza mwanamke ambaye hakuwa tayari kunisikiliza.

    

    Chipsi sio chakula kabisa jamani! Yani niliamka njaa imenibana mno. Tumbo jeupeee, linadai chakula tu. Moja kwa moja nikaenda katika meza. Nikalifungua lile poti. Ambalo tangu nilivyolipokea, sikutazama limewekwa nini. 


     Yule binti alinitengea upaja wa kuku, na lile pilau aliliweka kachumbari yenye kabichi. Kiukweli kachumbari ya aina hiyo ndiyo ugonjwa wangu. Hata mke wangu ndiyo ambayo hupenda kuniandalia. Nilikaa na kuanza kula. Akili ikawa inamkumbuka sana wife. Nikatafakari kumpigia. Japo mchana nilifanya hivyo kwa kurudia mara tatu na simu yangu hakuipokea.


    Hata kwa muda huo ambao nilimpigia tena, bado mke wangu hakuipokea simu iliyoita mpaka ikakata. Nilikuwa natamani kumpigia mama yake kumueleza kuwa binti yake yuko njiani, ama kama amefika basi nijue ikiwa amefika salama. Lakini nikawaza safari hiyo haikuwa njema, ni bora niache mpaka pale ambapo nitapigiwa, na kupewa mashtaka yangu, kisha ndiyo ikibidi, nianze kujitetea.


     Nikiwa nipo mwenyewe nikichezea tu simu kwa kupitia posts mbalimbali mtandaoni, nikasikia mlango wangu unagongwa. Ilikuwa yapata saa moja kasoro. Nikawaza huenda ni mke wangu ameamua kurejea nyumbani na labda hakwenda kokote. Niliwaza hivyo kwa sababu sikuwa na mgeni yeyote ninayemtegemea kwa siku hiyo.


    Nilipoufungua mlango, nikakutana na yule binti, jirani. Aliponiona tu akawahi kunitolea samahani. Alikuwa amesimama mlangoni huku amefunga kanga tu ya kifua. Kiukweli nilikuwa sijihisi uhuru kwa namna alivyokuwa amenisimamia. Sikupenda pia. Kama mtu yeyote angetokea na kutukuta, lazima tu kichwani kwake angeweka tafsiri mbaya ya anachokishuhudia.


     Nilimjibu, "Bila samahani!" Nikaweka utulivu kumsikiliza. Yule binti akasema umeme nyumbani kwake umezima. Na sio kwa sababu umeisha, lakini kuna kitu katika mita huwa kinafyatuka. Na huko katika mita pako juu kidogo, yeye kwa kimo chake hawezi kufikia. Hivyo kama sitajali, niongozane naye niende kumsaidia. Kumsaidia kukifyatua hicho kitu!


   Mpendwa msomaji, kabla haujanilaumu kwa jibu ambalo nilimpa binti huyo, naomba tukumbuke kwa pamoja kuwa, mpaka muda huo tulishakula pilau la watu ambalo tuliandaliwa. Usiseme hatukuwa pamoja mpendwa msomaji. Wewe pia uliniunga mkono nilivyokuwa nikisifia limewekwa kuku na kachumbari. Tena kachumbari ya kabichi. Lakini kingine, yule binti kweli ni mfupi. Mimi alikuwa kifuani hanifikii. Alikuwa ana kila sababu za kuupata msaada wangu. Hivyo nilikubali. Nilikubali kuongozana naye.


    Nilifunga mlango, tukaenda pamoja mpaka kwake. Mita yake ilikuwa kwa ndani. Na kwa sababu umeme haukuwepo, alitumia tochi ya simu yake kumulika. Yeye mbele, mimi nyuma. Na nilijitahidi kumfuata huku nidhamu yangu ikiwa ya hali ya juu kweli kweli. Sikutaka macho yangu yatazame chochote zaidi ya pale ambapo hatua za miguu yangu zilipokuwa zikipakanyaga.


    Niliingia ndani mwake. Tukawa tuko wawili tu ndani ya kiza kile chenye mwanga hafifu wa tochi ya simu. Akanionesha ilipo mita. Ni kweli ilikuwa juu sana. Hata mimi nilihitaji kupata stuli ndogo ili nipande nipafikie. Alipotaka kunishikia. Ili isije ikaniangusha, hiyo stuli, nikamkatalia. Maana ingemfanya awe karibu yangu sana. Hilo lingekuwa kama kumkaribisha shetani katikati ya uwanja wa vita.


       Lakini, ikawa tofauti kabisa yani na ambavyo yalikuwa mawazo yangu. Nikawa nahisi huenda yale ambayo mke wangu alikuwa akinisimulia kuhusu binti huyo ni habari tu za kunitia hofu labda ili nisizoeane naye. Wala hakuwa na tabu. Taa ilivyowaka nikakuta kuna kitabu cha riwaya juu ya meza yake. Nikamuuliza ikiwa anapenda kusoma fasihi. Akanijibu ni ulevi wake. Wala hakuleta kashikashi yoyote ile kwangu. Tena alikuwa anaongea kwa aibu mno. Akanitajia waandishi wengi ambao hata mimi walikuwa katika orodha ya watu ninaowasoma. Baada ya hapo akanishukuru sana na kunitoa mpaka mlangoni.


     Nikiwa narejea kwenda kwangu niliwaza sana. Nikatubu kwa Mungu wangu namna ambavyo nilikuwa ni mtu wa kumuwazia mabaya mwanadamu mwingine. Hapohapo pia nikamlaumu wife kimoyomoyo.. kwa sababu alinipa habari ambazo zikawa zinanifanya nimtazame kwa ubaya mtu asiye na hatia yoyote. 


    Nilipofika ndani, yale maongezi kuhusu vitabu kule kwa jirani yakanipandisha mzuka sana wa kutafuta na mimi cha kusoma. Nina kajimaktaba changu kidogo pale ndani. Japo vyote nilikuwa nimevimaliza, nikachagua kukichukua kimoja na kukirudia. Ila, hata kabla sijafika ukurasa wa nne wa kitabu hicho, mlango ukagongwa tena.


   Haraka niliwahi kwenda kuufungua. Ni jirani. Jirani kwa mara nyingine. Jirani alikuwa ameshika rundo la vitabu. Amevikumbatia. Vingi mnoo. Nikamuuliza vya nini. Akaniambia amekuja navyo ili nichague ambavyo nitavipenda. Nilipotaka kumpokea. Akasema niache tu. Kisha akaomba nimkaribishe.


    Ajabu ni kwamba, kabla hata sijamkatalia ama kumkubalia, alinipita haraka mlangoni na kuingia ndani. Akaenda na vile vitabu mpaka katika meza na kuvibwaga.

Hayo yote hayakuwa na tabu kwangu, kuleta vitabu, sijui kuingia ndani... Vyote vilikuwa ni sawa tu japo sio kivile. Ila kilichokuwa kikinipa wakati mgumu, ni ile kanga yake mwilini.

Vile alivyokuwa mwanzo, ndivyo alivyokuja kwa mara ya pili!


ITAENDELEA.


😄😄😄 haya jamani jirani kama jirani inaendelea,tuendelee kufuatilia tuone yaliyojiri mbele ila Abyas unaandika bwana weee


Naomba vitabu vyako vyote vya hardcopy vinifikie


Marm'z Relationship Hub  0710474782

Comments

Popular posts from this blog