Simulizi: JIRANI KAMA JIRANI!
Imeandikwa na : Abyas Mzigua
Sehemu ya kwanza
Hapa tunapoishi ni sehemu yetu ya kwanza tangu tufunge ndoa mimi na mke wangu. Tupo inatimu miaka mitatu sasa. Kiukweli sifikirii kuhama kabisa kwa sababu mama mwenye nyumba ni 'mzungu' vibaya mno.
Kwanza haishi hapa. Hakai kabisa eneo hili. Halafu ukifika muda wa kodi, anaweza akakuachia mwezi mzima wa kujipanga ikiwa tarehe imeshagonga na huna hela ya kumlipa. Sidhani kama kuna pepo nyingine mpangaji angetamani kuipata hapa duniani zaidi ya hii! Sidhani!
Lakini, pamoja na yote hayo, kipo kitu kimoja kinachonipa wakati mgumu mno. Na labda nianzie mbali kidogo ili muweze kunielewa vizuri...
Nyumba zetu hapa zipo tatu. Nyumba tatu kwenye uzio mmoja. Yani kiufupi tupo wapangaji watatu.
Ukiacha mimi na mke wangu, nyumba nyingine anaishi jamaa ambaye yeye kuonekana ni mwezi baada ya mwezi. Sijui ni mtu mwenye kazi gani maana hata mazoea na mtu hana. Mara chache tu huwa anakuja msichana wake ambaye naye pia hakai sana. Kidogo huyu msichana huwa namuona walau anasalimia ukikutana naye.
Sasa ukiacha huyo, kuna jirani mwingine huyo, naomba nilistahi tu jina lake. Siwezi kujua yupo kwenye orodha ya wafuasi wako, au pengine hata kuna watu wanamjua. Lisije likazuka balaa!
Huyu jirani ni binti, tena binti mwenye makamo madogo sana. Ni kasichana tu ambacho naamiini hata kwa umri hakinikuti.
Kipindi nahamia hapa, nilikuwa nakaona kakitoka asubuhi na kurudi jioni. Kipindi hicho ofisini yangu ilipata tabu kidogo nikawa niko nyumbani tu. Ndiyo maana nilikuwa namuona. Lakini baadaye nilikuja kushangaa tu yupo, haendi popote. Ni kachangamfu sana kwa kweli. Kanamuita mke wangu dada. Na mimi kananiita shemeji.
Niwe mkweli, mimi sio mtu wa mazungumzo kivile. Na kwa kuiheshimu ndoa pia, nikawa najitahidi kufupisha maongezi na binti huyo.
Ikiisha salamu baina yetu, kila mtu na mambo yake.
Ni wife ndiye ambaye alianza kuniletea habari kuhusu yule binti. Nadhani mlio kwenye ndoa ama mahusiano ya kuishi pamoja mnalielewa hili. Mkikaa kuna muda mnakosa vya kuzungumza, mnaanza kuongelea mambo ya watu yasiyowahusu.
Akawa ananiambia kuwa yule binti ni kicheche sana. Alisema, wakati nikiwa kazini, amemuona kamuingiza muuza duka fulani sijui, mara kuna mwanaume wa mama nani huko, mume wa mtu, naye kaingia humo ndani. Mimi kazi yangu ikawa ni kuitikia tu na kusikitika. Nilikuwa naamini hakuna linalonihusu wala kuja kunihusu mbeleni.
Na taarifa hizo zikawa zinazidisha tahadhari yangu dhidi ya yule binti. Nikawa namsalimia lakini najitahidi hata usoni simtazami kwa muda mrefu. Japo alikuwa ni mtu mwenye bashasha na kutamani walau kuwe kuna kauli mbili tatu baada ya salamu hiyo. Mimi sikuliruhusu hilo litokee. Hata kidogo.
****
Sasa kuna kipindi, mwaka juzi ile mwishoni, mimi na mke wangu tulipishana kidogo kauli. Na ilikuwa ni kuhusu wazazi wake tu. Nisingependa kuirudia. Nikiri kwamba aliyeteleza kwenye hilo ni mimi. Wife hakupenda kwa kweli. Alilia sana. Nilijaribu kumbembeleza na kumtuliza lakini hakuwa tayari kunisikiliza.
Mwisho kabisa akaomba nimrejeshe kwao. Alikuwa anasema maneno mengi ya lawama. Kwamba namdharau kisa hana kazi, kisa familia yao iko chini. Malalamiko yalikuwa ni mengi kutokana na kauli moja tu. Sijitetei, lakini naamini ilikuwa ni kauli ya kuzungumzika tu kisha mambo mengine yaendelee. Kwa sababu hata vikombe vilivyopangwa kabatini navyo hugongana.
Nilitumia busara. Niliona kuendeleza mzozo linaweza kuwa jambo baya zaidi kwetu. Nikamruhusu mke wangu aende kwao. Tena nilitaka kumpeleka mwenyewe. Lakini alinikatalia katukatu. Ikabidi nimpe nauli na awe huru kwa kile alichokiamua. Japokuwa moyoni nilikuwa nina fikra zangu baada ya muda ningemfuata na kumrejesha. Kwa sababu namjua. Ni mtu mwenye hasira sana. Ila huwa zinapungua kadiri siku zinavyotembea.
Siku iliyofuata ikawa imekuja na upweke. Mke wangu aliondoka akaniachia nyumba yote peke yangu. Nakumbuka niliomba ruhusa ofisini ili nitumie muda wa kutosha kujaribu kumbembeleza, lakini hakuna ambacho kilibadilika. Hivyo kutwa nzima nikawa nimebaki mimi mwenyewe nikitazama na kuta. Kuta ambazo kuna wakati nilikuwa nahisi kama vile zinanizomea kwa namna nisivyojua kuuchunga ulimi wangu!
Kukaribia mchana, yule jirani akaja. Yule jirani wa kike ambaye mwanzo nilikueleza kwa uchache kuhusu yeye. Enhee... Huyohuyo!
Alikuja kumuulizia mke wangu, nikamjibu hayupo. Akataka kujua ikiwa angerejea. Nami nikafanya kosa kubwa sana la kumjibu kuwa amesafiri. Sikufunguka sababu ya safari wala nini. Lilikuwa ni neno moja, lakini mpendwa msomaji taratibu huko mbeleni utakuja kunielewa ni kwanini nasema kosa kubwa sana.
"Eh! Shem jamaaani, pole... Ndiyo maana umepooza mwenyewe!" Aliniambia hivyo huku bashasha likiwa limemtawala. Mimi nilijibu tu "Ahsante!" Halafu ukawa ndiyo mwisho wa maongezi yetu.
Nilirudi zangu ndani. Baadaye kidogo, kama saa sita hivi, nikapiga simu kwa bodaboda na kumuagiza aniletee chipsi pamoja na soda. Sijui kuchemsha hata chai yangu ndugu'enu mwenzenu.... Sijui mimi wallahi!
Na wife sio kwamba hatambui hilo, anaelewa vizuri. Na bila shaka alikuwa anafahamu kabisa adhabu ya kuniacha peke yangu haiwezi kuwa nyepesi!
Chakula nilichoahiza kililetwa, Nilikula, nikashiba. Nikaweka filamu na kuanza kuitazama. Unadhani mawazo yalikuwa hapo kwenye filamu? Nilikuwa mbali mno. Nilikuwa nawaza namna ambavyo atafika nyumbani kwao na kuulizwa nini kimetokea.... Nikapata wasiwasi wa kitu gani ambacho angekwenda kuongea...
Basi kausingizi hapohapo kakanipitia.
Nilikuja kukurupuka, kwa kusika mlango ukigongwa. Nikamuitikia mgongaji na kuwahi kwenda kuufungua.
Alikuwa ni jirani yetu, yule binti, amesimama huku ameshika poti mkononi mwake...
"Shem, nimepika pilau, nikaona nikuletee kwa sababu dada hayupo...!"
Nilitaka kukataa. Kwa kumjibu nimeshakula chipsi. Tena kwa bahati nzuri karatasi ya mabaki haikuwa mbali, nikamuonesha uthibitisho kwa kunyooshea kidole.
Akanijibu huku akicheka, "Hahaha! Basi haina tabu shem, utakula tu hata usiku! Bado kitakuwa cha moto!"
Kwa kweli hapo sikuweza tena kupindua neno. Nilikipokea chakula kile na kushukuru. Nikaingia nacho ndani...
Na huo, rasmi, ukawa ndiyo mwanzo wa yote!
ITAENDELEA.
Haya jirani kama jirani tuendelee kufuatilia tujue nini kitajiri 😄🤔
Marm'z Relationship Hub 0710474782
https://maishakitaaonlinetz.blogspot.com/?m=1


Comments
Post a Comment